Katika ujumbe wake wa “Urbi et Orbi” kwa Sherehe ya Pasaka tarehe 5 Aprili 2026, Baba Mtakatifu Leo XIV amesisitiza kuwa Ufufuko wa Kristo ni ushindi wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, akibainisha kuwa nguvu ya upendo wa Mungu ndiyo chemchemi pekee ya amani ya kweli inayoweza kukomboa ulimwengu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.
Papa ametoa mwito wa dharura kwa jamii ya kimataifa kuacha mazoea ya vita na chuki, akihimiza ujenzi wa amani inayosimikwa katika majadiliano, ukweli, na uwazi badala ya kutafuta faida binafsi au kutawala wengine kwa mabavu. Akikazia kuwa Msalaba wa Kristo ni kielelezo cha mahangaiko ya binadamu yanayoshindwa na mwanga wa Ufufuko, amewaasa wenye silaha kuziweka chini na kufungua nyoyo zao kwa wongofu wa ndani.
Hatimaye, Baba Mtakatifu ametoa mwaliko wa kipekee kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuungana naye katika Mkesha wa Kuombea Amani Duniani utakaofanyika Jumamosi tarehe 11 Aprili 2026, katika Uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, ikiwa ni mkesha wa Pasaka 2026