Kila Siku za Wiki Asubuhi
Sakeramenti ya Kitubio ni Sakramenti inayotuondolea dhambi tulizotenda baada ya ubatizo. (Kat. Tec 189)
SAKRAMENTI YA KITUBIO
Sakramenti ya Kitubio (Maungamo) pia hujulikana kama Sakramenti ya Upatanisho, ni moja ya Sakramenti za Uponyaji pamoja na Sakramenti ya Mpako Mtakatifu. Sakramenti ya Kitubio ni tendo la neema ambapo mkristo mbatizwa aliyeteleza hurejeshwa katika urafiki na Mungu na Kanisa baada ya kutenda dhambi baada ya Ubatizo. Msingi wa sakramenti hii unapatikana katika mamlaka ya Kimungu ambayo Bwana wetu Yesu Kristo mwenyewe aliwapa Mitume wake alipowavuvia Roho Mtakatifu na kusema, “Pokeeni Roho Mtakatifu. Wowote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wowote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa” (Yn. 20:23). Katika aya hii, Yesu anaweka wazi kuwa amewashirikisha wanadamu (Maaskofu na Mapadre) uwezo wake wa kusamehe dhambi, si kwa nguvu zao wenyewe, bali kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, ili kila anayetubu kwa dhati aweze kusikia sauti ya hakika ya msamaha wa Mungu kupitia Kanisa lake.
Ili kupokea sakramenti hii vizuri, mkristo mbatizwa anapaswa kufuata hatua kuu tano, ambazo ni: kuchunguza dhamiri, kutubu kwa dhati, kudhamiria kutorudia kutenda dhambi, kuungama mbele ya Padre, na kutimiza malipizi. Maandiko Matakatifu yanatukumbusha kuwa, “Tukiziungama dhambi zetu, yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote” (1 Yn. 1:9). Tendo hili si la kisheria tu, bali ni kama simulizi la Mwana Mpotevu (Lk. 15:11-32), ambapo Baba mwenye huruma anamkimbilia mwanawe aliyepotea na kumrejeshea hadhi yake. Na hivi kumbe, kupitia Sakramenti ya Kitubio (maungamo), mkristo anapokea amani ya moyo na nguvu mpya ya kiroho ya kushinda vishawishi, akijua kuwa neema ya Mungu ni kuu kuliko kosa lolote lile atendalo mwanadamu.