Ekristi Takatifu: Njioni Tumuabudu

“Huu ndio Mwili wangu utakaotelewa kwaajili yenu na hii ndiyo damu yangu itakayomwagika kwajili yenu” , “Fanyeni Hivi kwakunikumbuka mimi” (Luka 22:19-20)

MAANA YA EKARISTI : Tunamwuabudu Ekaristi Takatifu Kila Alhamish 

Ekaristi Takatifu Ni nini?

Neno Ekaristi asili yake ni lugha ya Kigiriki “Eucharistein” likimaanisha shukrani. Ekaristi Takatifu ni sadaka ya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo. Pia huitwa Misa Takatifu, karamu ya Bwana, kumega mkate, kusanyiko la Kiekaristi, ukumbusho wa mateso kifo na ufufuko wa Bwana, Sadaka Takatifu ya Misa, Liturujia Takatifu, Sakramenti Takatifu sana ya Altare na Komunyo Takatifu. Ni ishara ya umoja na kifungo cha mapendo, karamu ya Pasaka ambamo waamini humpokea Kristo na roho hujazwa neema na kupewa amana ya uzima wa milele. (KKK 1322 – 1323, 1409).

Ni Sakramenti ya umoja na upendo, kimsingi, Ekaristi ni kiini kamili katika Kanisa, na Kanisa haliwezi kitu pasipo hiyo. Kwasababu ni Kristo mwenyewe anayejitoa kweli kama sadaka kwa ajili ya Kanisa katika Ekaristi Takatifu na ni katika Ekaristi Kanisa hufikia uhalisia wake wa juu wa asili yake, yaani, kuwa linaonekana, la daima, na alama wazi ya neema ya wokovu ya Mungu iliyopo duniani kupitia Kristo. Pia Ekaristi ni mojawapo kati ya Sakramenti saba za Kanisa ambazo ni alama wazi zilizowekwa na Yesu Kristo Mwenyewe ili kutuletea neema ya wokovu.

Ekaristi ni Sakramenti inayokamilisha tendo zima la kumwingiza Mkatekumeni katika ukristo. Tofauti na Sakramenti zingine Ekaristi ni Kristo mwenyewe katika maumbo ya mkate na divai. Mtakatifu Thomaso wa Akwino anasema Sakramenti zingine zote zimeimarishwa kwa Sakramenti ya Ekaristi.

Sakramenti ya Ekaristi Takatifu iliwekwa na Yesu Kristo mwenyewe siku ya Alhamisi kuu, wakati ule wa karamu ya mwisho aliyokula pamoja na wanafunzi wake. Uwezo wa kuugeuza mkate kuwa mwili wake na divai kuwa damu yake alitoa Yesu Kristo mwenyewe siku hiyo kwa Maaskofu na Mapadre wote wa Agano Jipya kwa njia ya mitume (Lk 2:19; 1Kor 11:23-25).

Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican unathibitisha kwamba, Ekaristi ni “Chemchemi na kilele cha maisha yote ya Kikristo”.

Hivyo Ekaristi inaunda Kanisa na Kanisa linaitengeneza Ekaristi, na ndimo linamochota nguvu ya kiroho. Kumbe hakuna jumuiya ya Kikristo inayoweza kujengwa na kusimama imara bila adhimisho la Sakramanti Kuu ya Ekaristi Takatifu. Katika Ekaristi Takatifu fumbo la Ukombozi wetu linawekwa hai na kufikia kilele katika sadaka ya Bwana, kama inavyotamkwa katika maneno ya konsekrasio:

“Huu ndio Mwili wangu utakaotolewa kwa ajili yenu na hii ndiyo Damu yangu itakayomwagika kwa ajili yenu”, “Fanyeni hivi kwa kunikumbuka mimi” (Luka 22:19-20). Sisi sote tunaalikwa kwenye karamu hii ili tuweze kushiriki katika uzima ule ule wa Kristo.  “Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake. 

Ni hasara kubwa sana kutopokea Ekaristi kwa kuwa umejiwekea vizuizi, umejifungia. Wale wasiopokea Ekaristi nawasihi fanyeni bidii kubomoa kuta za vizuizi mpokeeni Ekaristi, ili Muungane na jamii ya waamini katika Ekaristi na kuwa kweli wakristo. Tukiwa na tofauti katika familia, katika nafasi za kazi, katika vyama vyetu vya siasa, tuiangalie Ekaristi ili iwe sababu yetu ya kuthaminiana, kuheshimiana na kupendana kwa kuwa Ekaristi inatuunganisha inatufanya tuwe wakristo kweli kweli. 

Tumsifu Yesu Kristo katika Sakramenti kuu ya Altare.